Monday 7 May 2018

Utata katika kufasili ya dhana ya neno.

Utata katika kufasili ya dhana ya  neno.


Fasili ya neno.
TUKI, (2004: 305) katika kamusi ya Kiswahili sanifu wanadai kuwa neno ni mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au kuandikwa pamoja na kuleta maana.
 
Katamba,(1994:38) anasema kuwa neno ni kipashio kidogo cha maana katika lugha ambacho kiana dhima kisarufi. Anaendelea kusema kuwa, neno linaweza kusimama pekee yake na kuleta maana bila kupachikwa vipande vingine.
Kwa mfano, neno childish (utoto) linaweza kutenganishwa na kubaki child (mtoto) na neno hili linatumika kiupwekeupweke kwa sababu ni neno linalojitegemea lakini hatuwezi kutenganisha kipande {-ish}kikasimaa pekee yake na kuleta maana.
Habwe & Karanja, (2007:71) wanafafanua kuwa neno ni kipashio cha kiisimu kinachoundwa na mofimu moja au zaidi. Wanaendelea kueleza kuwa dhana ya neno ni tata mno hasa katika kubainisha neno na vipashio vingine katika lugha. Kwa mzawa wa lugha yoyote ile, ni rahisi kutambua neno kutokana na vipashio vingine kwa kutumia ujuzi na mazoea ya matumizi ya lugha husika. Kwa mfano, miundo ifuatayo hutambuliwa na mzawa wa lugha ya Kiswahili kuwa ni maneno ya Kiswahili: 
                                              (i)Wanalim
                                              (ii) mwanfunzi 
                                              (iii) shuleni
                                               (iii) kalamu
Hivyo basi, kutokana na maana hizo tunaweza kusema kuwa neno ni kipashio cha lugha kinachoundwa na mofu moja au zaidi ambayo inaweza kusimama pekee yake na kuleta maana katika lugha mahususi. Ingawa dhana hii ya neno imezua utata kutokana na watalaamu mbalimbali kuibuka na vigezo tofauti tofauti vya kufasili dhana hii na mipaka yake. Tukimchunguza Mdee, (2010:5) anadai kuwa kuna vigezo vikuu vitatu vya kufasili dhana hii ambavyo ni kipashio huru kisichogawanyika, maana ya neno kiothografia na maana ya neno kisarufi.
Hata hivyo, kwa mwanaisimu huwa ni vigumu kutoa kijelezi kamili cha dhana ya neno na badala yake fahiwa mbalimbali za dhana hii zimetumika kiutendaji. Baadh ya fahiwa zilizotumika kueleza dhana yaneno ni ,midhihiriko ya neno, muundo wa neno, neno kisarufi. Hapa tutajikita kuzungumzia fahiwa mbili za dhana ya neno yaani midhiriko ya neno na muundo wa neno kama ifuatavyo:

  1. Midhihiriko
Udhihirikaji ni utokeaji katika utendaji halisi wa kipashio cha kiisimu kilicho dhahiri. Dhana ya neno hujitokeza kiutendaji na midhihiriko kadhaa, udhihirikaji wa neno huweza kujitokeza kupitia dhana zifuatazo:
Udhihirikaji kileksimu; leksimu ni kipashio kidogo kabisa cha msamiati ambacho kina uwezo wa kusimama pekee yake kama kidahizo. Kwa upande mwingine kidahizo ni msamiati ambao huorodheshwa katika kamusi. Kwa kurejelea leksimu, midhihiriko ni miundo mbalimbali ya leksimu na huwa na maana ya kimsingi ingawa huenda ikatamkwa na kuendelezwa kwa njia tofauti (Habwe & Karanja, 2007:72). Kwa mfano kutokana na leksimu “lima” tunaweza kuwa na midhihiriko ifuatayo:
Lima----->lima, limiwa, alilima, hulima, mkulima, n.k
Matamshi tofauti na jinsi yanavyoandikwa; midhihiriko hii inarejelea maana sawa ya kimsingi ingawa inatamkwa na kuendelezwa kwa njia tofauti tofauti. Vile vile dhana ya midhihiriko katika neno kwa mujibu wa Saluhaya, (2010:79-80) anasema kuwa neno huweza kudhihirika kwa matamshi ambayo ni tofauti na linavyoandikwa. Pia Kihore na wenzake,(2003:43) anadai kuwa katika lugha ya Kiswahili kuna maumbo machache yasiyokuwa na uwiano wa kimatamshi na kimaandishi. Kwa mfano, maneno kama vile ng’e, mba, mbu, ngwe, nje na mbwa ni baadhi ya maneno ambayo huandikwa tofauti na jinsi yanavyoandikwa. Pia Saluhaya, (2010) anadai kuwa sababu zinazofanya maneno yatamkwe tofauti na jinsi yanvyoandikwa ni kama zifuatazo:
  1. Athari za usanifishaji uliofanywa na wazungu; kazi ya usanifishaji iliyofanywa na waingereza ambao asili ya lugha yao haihusiani na lugha ya Kiswahili. Wazungu ndio walioteua othografia ya Kiswahili chini ya mwingereza Profesa Fedrick Johnson ambaye ndiye aliyesimamia usanifishaji wa othografia ya Kiswahili akiwa kama katibu wa kamati ya usanifishaji wa lugha ya Kiswahili iliyoundwa mwaka 1930.
  2. Upungufu wa herufi za kuwakilisha sauti za lugha ya Kiswahili; lugha ya Kiswahili kama ilivyo kwa lugha nyingine nyingi haijitoshelezi katika herufi za kuwakilisha sauti zake. Hii ni kwa sababu lugha ya Kiswahili inatumia mfumo wa maandishi uliobuniwa kwa ajili ya lugha nyingine tofauti na lugha ya Kiswahili.
  3. Tatizo la kiothografia; tatizo hili husababishwa na baadhi ya maneno kuwakilishwa kimaandishi na herufi pungufu kuliko ilivyo katika matamshi yake. Kwa mfano maneno kama vile nchi, nje, nne, ni baadh ya maneno ambayo yana herufi pungufu.
  4. Athari za kimazingira; mara nyingi matamshi ya wasemaji wa lugha huweza kuathriwa na mazingira mbalimbali waliomo kiasi cha kuwafanya wasiweze kutamka maneno kama yalivyoandikwa.
Kwa hiyo, tukichunguza kwa kina dhana hii ya midhihiriko tunaweza kugundua kuwa midhihiriko katika neno hujitokeza kupitia utokeaji katika utendaji halisi wa kipashio cha kiisimu kilicho dhahiri. Vile vile neno huweza kudhuhirika kupitia matamshi ambayo ni tofauti na jinsi ambavyo huandikwa. Hivyo midhihiriko ya neno mara nyingi hujikita katika kuangalia maana za msingi za maneno husika.
  1. Muundo wa neno
Habwe & Karanja, (2007:73) wanafafanua kuwa njia nyingine ya kutambulisha neno ni kwa kurejelea miundo mabalimbali ya leksimu katika tungo kimaandishi au kiusemaji yaani kwa kuangalia muundo mahususi wa neno. Hivyo, kwa mfano katika kipengele cha midhihiriko, tumeweza kutoa mifano kama vile lima, limisha, mkulima, limiwa. Kwa upande wa muundo wa neno, maneno kama haya ni maneno manne tofauti licha ya kuwa yanarejelea maana moja sawa ya kimsingi. Miundo ya maneno katika lugha mbalimbali huwa kama ifuatavyo:
Muundo wa mofu tegemezi; katika muundo huu neno huwa limeundwa na sehemu kuu tatu ambazo ni viambishi awali, mzizi na viambishi tamati. Kila sehemu ya neno hilo huwa lina dhima yake kisarufi na kuwa sehemu kamili linalound neno hilo, ikitokea ukabadili sehemu mojawapo neno hupoteza maana ya msingi, kwa mfano,
  1. {Mwimbaji} mw-imb-a-ji
  2. {Anaimbisha} a-na-imb-ish-a
  3. {Watakapotuimbia} wa-ta-ka-po-tu-imb-i-a
Mofu kama hizi endapo zitasimama pekee yake haziwezi kuleta maana kamili bali hutegemea viambishi ili kukamilisha taarifa iliyokusudiwa.
Muundo wa mofu huru; katika muundo huu neno haliundwi na viambishi awali, mzizi na wala viambishi tamati bali kwalo huwa na mzizi au neno huru linajitosheleza kimaana pasipo kupachikwa viambishi. Mfano wa mofiu hizi ni pamoja na majina ya watu, majina ya mahali, majina ya miezi, majina ya nchi, na baadhi ya vielezi kwa mfano, Herman, Tanzania, Mwanza, Januari, polepole, wasiwasi, na maneno mengine yanayofanana na hayo.
Maneno kama hayo hapo juu ni mofu huru ambayo hayategemei viambishi vya aina yoyote na yanatoa taarifa kamili. Ikumbukwe kuwa maneno kama wasiwasi na polepole ni mofu huru kwani huwezi kuyagawa na yakabaki na maana ya msingi ile ile.
Muundo wa mofu ambatani; maneno haya huwa yanundwa na mizizi au mashina mawili tofauti tofauti yaliyounganishwa kwa pamoja kwa kuacha nafasi ama kutokuacha nafasi katika mizizi au mashina hayo ili kuwasilisha dhana moja kimaana. Aghalabu maneno haya huundwa kwa kuweka pamoja mizizi au mashina ya maneno mawili tofauti na kupelekea kibuka kwayo, mizizi au mashina hayo yaweza kuwa tegemezi au huru, kwa mfano, asikari kanzu, mwanajeshi, mwanahewa, bata mzinga, kipazasauti, kipimahewa, na maneno mengine kama hayo.
Kiukweli; maelezo kuhusu dhana ya neno ni tata, aghalabu huelezeka kutokana na vigezo mbalimbali vinavyotumika kufasili neno kuonekana ndicho kiini cha ugumu wa ufasili wa neno, pia tofauti za lugha huchangia kwa sababu lugha nazo hutofautikana kwa namna mbalimbali, wakati mwingine mizatamo tofauti tofauti huchangai pia kuifanya dhan hii kuwa ngumu, hivyo ni muhimu kwa wanafunzi wa kozi ya mofolojia kuelewa vigezo hivi kwa kuhusianisha mawazo ya watalaamu mbali mbali katika kujadili dhana hii ya neno. Kwa kuelewa dhana hii barabara itmwezesha mwana mofolojia kuweza kuyapanga maneno kutegemeana na vigezo vya uainishaji vilivyo elezwa hapo juu, ingawa kuna kigezo cha kisarufi hakija jadiliwa hapa kutokana na mawanda ya kazi yetu kuwa na kikomo cha vigezo vya midhihiriko na muuondo wa neno tu.

MAREJELEO
Habwe, J & Karanja, p.(2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers
Katamba, F. (1994). Morphology. London: Mac Millan Press Ltd
Kihore, Y.M, Massamba, D.P.B., Masanjila, Y.P. (2003). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu
(SAMIKISA) Sekondari na Vyuo. Dar es salaam: TUKI.
Mdee, s. (2010). Nadahria na Historia ya Leksikografia. Dar es salaam: TUKI
Saluhaya, M.C. (2010). Kiswahili 1 Nadharia ya Lugha. Dar es salaam: STC Publishers.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es salaam: Oxford University Press,
East Africa Ltd.

No comments:

Post a Comment