UHAKIKI WA RIWAYA YA KUSADIKIKA
UTANGULIZI
Katika
kujadili vipengele mbalimbali vya Fani na maudhui vilivyotumiwa katika riwaya
ya kusadikika iliyoandika na Shaaban Robert Washiriki hatukujikita zaidi katika
kujadili maana ya riwaya za wataalamu mbalimbali bali tuliweza kujadili kazi
hii kwa kuchambua vipengele vya fani na maudhui kutokana na masimulizi ya nchi
ya Kusadikika. Masimulizi ya kitabu kwa kifupi.
Riwaya
ya Kusadikika ni kitabu kinachoelezea
masimulizi ya nchi ya kusadikika ambayo mwandishi ameanza kwa kusimulia tukio
la kushitakiwa kwa Karama ambaye
ndiye Mhusika mkuu kwa tuhuma za kuihujumu serikali ya Kusadikika. Kwa maelezo
ya Waziri Majivuno aliwasilisha
mashitaka haya mbele ya Mahakama eti kwa sababu Karama alikuwa akitoa elimu ya
sheria ambayo kwa Mtazamo wa Waziri huyu alidai kuwa angewafanya raia wa
kusadikika kuelewa haki zao ambako kungepelekea wananchi hao kutotii serikali
au kwa namna nyingine kungekomesha unyanyasasaji, uonevu na uongozi mbaya wa
watawala wa kusadikika na hivyo waziri
Majivuno alijawa hofu kubwa sana. Riwaya imeendelea kusimulia namna
mshitakiwa Karama alivyowasilisha utetezi wake mbele ya Mahakama ya Kusadikika
iliyoundwa na Mfalme na Madiwani. Karama aliwasilisha utetezi huo kwa
kuthibitisha jinsi serikali ilivyoshindwa kuthamini michango mbalimbali ya
wananchi wake kwa kuelezea historia wajumbe mbalimbali waliojitoa kwenda
kufanya utafiti wa namna ya kuendeleleza nchi yao. Masimulizi yake yaliwataja
hasa wajumbe 6 waliotumwa mipakani au pande zote 6 ambazo nchi ya kusadikika
inapakana nayo. Pande hizo niKaskazini,
Mashariki, Kusini, Magharibi, Mbinguni na Ardhini.
Hatima
ya wajumbe hawa ambao walikuwa
wazalendo waliishia Kifungoni pindi waliporejea kutoka walikotumwa. Mwisho wa
riwaya hii mwandishi anaelezea hukumu ya Karama ambapo Mahakama iliyoongozwa na
Mfalme ilivyomtoa hatia mtuhumiwa kwa kauli moja ya kuwa hana hatia na Mfalme
kuagiza wajumbe wote waliokuwa wanatumikia kifungo kufunguliwa na kulipwa fidia
kwa kunyanyaswa pamoja na jitihada zao.
Baada ya
muhtasari wa masimulizi ya nchi ya kusadikika niliweza kujadili vipengele
vinavyounda Fani na Maudhui ya kazi ya riwaya ya kusadikika kama ifuatavyo;-
Fani ni
ujuzi au Mbinu mbalimbali azitumiazo msanii kuwasilisha ujumbe au Fikra zake
kwa hadhira aliyoikusudia. Fani inaundwa na vipengele vya Mandhari, Wahusika,
muundo, Mtindo na Matumizi ya lugha. Maudhui ni jumla ya mawazo
yanayowasilishwa na msanii wa kazi ya kifasihi katika kazi yake. Maudhui
huundwa na vipengele vya Dhamira, Ujumbe, Falsafa, Migogoro, Mtazamo na
Msimamo. Uchambuzi wa Vipengele mbalimbali alivyovitumia mwandishi wa riwaya
hii ya Kusadikika ni:
Mandhari:
ambayo humaanisha mahali au sehemu ambayo tukio linafananyika. Mwandishi
ametumia mandhari ya Kufikirika ambayo haiwezi kujidhihirisha kwa macho ya
kawaida (haionekani) kwani ni nchi inayoelea angani. Pia ametumia mji wa sadiki
na mipaka au pande sita zinazopakana na nchi hii za Kaskazini, Mashariki,
Kusini, Magharibi, Ardhini na Mbinguni.
Wahusikani
mtu au watu, wanyama, na mimea anaotumia mwandishi katika kuwasilisha kazi yake
kwa hadhira iliyokusudiwa. Kwa kiasi kikubwa Mwandishi ametumia Wahusika ambao
aliowapa majina yanayosawiri tabia zao na wahusika ambao hawabadiliki badiliki
;-
Karama,
Huyu ni mhusika mkuu ambaye pia alikuwa Jasiri na Shujaa, Mwanasheria, Mzalendo
mtetezi wa haki na Mshitakiwa. Vilevile mhusika huyu alichorwa mwema kuanzia
mwanzo hadi mwisho.
Majivuno,
Waziri wa kusadikika, mwenye uchu wa madaraka, mwenye haiba, asiye na uzalendo,
kiongozi anayelindwa na Mfalme na asiye na shukurani. Mfalme, Kiongozi wa
kusadikika, Katili, Mjinga, mwenye tama ya uongozi, mkuu wa baraza la Mahakama.
Madiwani, Wasaliti, wakuu wa mahakama, waonevu, wakatili, wenye dhuluma na sio
wazalendo. Mudir wa sheria, mwanasheria wa serikali, Mjinga, msaliti na asiye
mzalendo. Buruhani, Mjumbe wa kaskazini, Jasiri, Mzalendo mpenda haki,
Mwanaharakati, Mfungwa na maskini. Msanii anasema “Hii ilikuwa safari ya
ujasiri iliyotaka uthabiti na matumaini, mwenye heshima, hodari na mwaminifu
alitakiwa ajitolee mwenyewe kwa safari hii” uk.12. Fadhili, Mjumbe aliyetumwa
mashariki, Jasiri, Mzalendo, mpenda haki, Mfungwa na maskini. “Mtu mwenye sifa
njema alitakiwa kujitolea mwenyewe kwa ujumbe wa mashariki na mtu kama huyu
alipatikana upesi sana kuliko ilivyokuwa ikitazamiwa” uk.16. Kabuli, Mjumbe wa
kusini, jasiri, Mzalendo, Mpenda haki, Maskini na mfungwa. Auni, Mjumbe wa
Magharibi, Jasiri, Mzalendo, Mpenda haki, Mwananchi wa kawaida na mfungwa. Sapa
na Salihi, walikuwa vipofu, wananchi wa magharibi, Sapa alikuwa mwenye tama na
wivu, Sapa alikuwa mpole, Sapa aliomba upofu. Radhaa, mjumbe wa mbinguni,
Jasiri, mzalendo, mpenda haki, Mfungwa na Maskini. Amini, mjumbe wa ardhini,
Jasiri, mpenda haki, mzalendo na mfungwa. Wahusika wengine ni wananchi, bwana
Taadabuni, katibu wa serikali, bwana Komeni, Amiri jeshi, bwana fujo, mlinda
hazina, bwana Baromini na wananchi wa pande zingine.
Muundo,ni
namna au jinsi mwandishi anavyopangilia visa na matukio katika kazi yake ya
kifasihi. Mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja ambapo katika mpangilio wa
masimulizi ameanza mwanzo wa kisa kwa kuonesha jinsi mashitaka
yalivyowasilishwa, kukafuatiwa na utetezi wa mshitakiwa au kile mwandishi
alichokiita maombezi mbele ya Mfalme na Madiwani kwa kusimulia historia ya
kusadikika kupitia wajumbe sita waliotumwa pande sita na kuishia kifungoni kama
sehemu ya pili ya kisa na hatimaye alimalizia kwa kuelezea hukumu ya kesi ya
Karama ambapo Mfalme na Madiwani walionesha kuwa mtuhuma hakuwa na hatia na
kufunguliwa kwa wajumbe sita na kuachiwa huru huku Mfalme akiamuru walipwe
fidia.
Mtindo.Ni namna mwandishi anavyoiumba kazi yake ya
kifasihi. Mwandishi Shaaban Robert ametumia mitindo mbalimbali katika kazi hii
ya riwaya ya kusadikika kama vile, ametumia maswali hasa katika sehemu ya
mwisho ya kitabu, ametumia dayalojia kati ya Sapa na Salihi uk. 29, ametumia
masimulizi kwa kiasi kikubwa katika kazi hii ambayo kwake ndio mbinu kuu pamoja
na matumizi ya nafsi ya pili na tatu umoja na nafsi ya tatu wingi sehemu kubwa
ya riwaya.
Lugha.
Mwandishi ametumia lugha ngumu ambayo si rahisi kueleweka kwa msomaji kutokana
na kutumia misamiati isiyoeleweka. Hali hii ya kutumia lugha ngumu ililengwa
kukwepa makucha ya wakoloni. Mfano wa misamiati hiyo ni sudusi, takirifu,
kafaungo, hutasawari, akapatilizwa, ali, kujikagajuu, Kuyabisika, kujikaga,
Kadura n.k. Pia mwandishi ametumia vipengele vya Tamathali za semi ambazo ni ;-
Methali. Kitanda usichokilalia hujui Kunguni wake. Msiba wa kujitakia hauna
kilio. Lila na fila hawatangamani. Misemo. Kumtosa mshitakiwa katika bahari ya
maangamizi. Tashibiha. Umri wake mkubwa ulizofanya nywele zake za kichwani kuwa
nyeupe kama fedha. Uso wa kipofu wa kwanza ulikuwa na furaha kama bwana harusi.
Alikuwa na tabia ya kuficha siri kama kaburi lifunikalo maiti. Anamaneno kama
kitabu Tashihisi. Giza limezalo nuru na ufupisho uoni wa macho. Wakati una
mabawa kama ndege uk. 11. Jina la Kitabu (KUSADIKIKA). Jina la kitabu
linasawiri yaliyomo katika riwaya hii kwani limetokana na neno “sadiki”
likimaanisha “Amini” hivyo linaweza kusemwa kuwa ni kuaminika. Mwandishi
anatuonesha kuwa Wasadikika ni wajinga kwani hawakujihusisha na uchambuzi wa
masuala yake waliishia kuamini na kukubali kila jambo mwandishi anasema “Imani
ya Kusadikika ni nguzo imara ya majengo ya utawala wa Wasadikika” wakati
mataifa mengine yalipojifananisha kwa mambo kama vile enzi, uwezo na fahari
nyingine taifa la kusadikika lilijivuna kwa sababu ya kusadiki mambo yaliyotoka
vinywani mwa watu wake” uk. 4-5. Kwa washiriki wa uchambuzi huu wanakiri kuwa
kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kuchambua haya katika vipengele vya fani na
maudhui alivyotumia msanii Shaabani Robert katika riwaya ya Kusadikika ingawa
si vyote vilivyotumika katika vipengele hivi tumeweza kuviainisha. (rejea ya kitabu)
MAUDHUI.
Maudhui
ni jumla ya mawazo aliyonayo msanii katika kazi yake ya kifasihi, Kipengele cha
maudhui kinaundwa na ujumla, dhamira, migogoro, falsafa, Msimamo/Mtazamo.
Dhamira mbalimbali Dhamira kuu ni Ukombozi: Dhamira hii ndio kuu katika riwaya
ya kusadikika iliojikita kwenye ukombozi wa kifikra na ukombozi wa kisiasa.
Mwandishi amemtumia mhusika karama aliyeanzisha elimu ya sheria yenye lengo la
kuwezesha wananchi ili wawezekushiriki katika mambo mbalimbali ya nchi.
Ukombozi wa kisiasa unarejelea harakati zilizoongozwa na Karama na wajumbe sita
zenye lengo la kuleta mabadiliko katika nchi ya kusadikika kuhusu haki na
uongozi (viongozi). Msanii anasema “Kwa nini wanasiasa wa kusadikika
hawakuwaacha kama Karama kujishughulisha na mambo yaliyowapita vimo vyao”
Matabaka. Hali ya wahusika kuwa na hadhi au makundi au madaraja tofauti
tofauti. Katika riwaya ya kusadikika ameonesha matabaka ya namna mbalimbali
kama;- Tabaka la viongozi na wananchi, matajiri na wasomi na wasio wasomi na
wenye haki na wasio na haki. Katika kudhihirisha matabaka haya mwandishi
ameeleza kwa mifano baadhi ya maeneo haya anasema “Sheria za wasadikika
zilikuwa hazimuamuru mshitakiwa kujitetea juu ya ushahidi wa mshitaki. Aghalabu
mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa
mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu
ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka salama ya watu wadogo ilikuwa
kidogo sana katika nchi ya kusadikika” uk.7. Uongozi Mbaya. Mwandishi
amedhihirisha hili kwa kuwatumia wahusika waziri Majivuno, Wafalme, Madiwani na
matajiri ambao ndio waliochorwa kwa taswira ya kuwa Wanahaki zaidi kuliko
wananchi wa kawaida. Tunapozungumzia uongozi mbaya ni hali ya utawala
kutowajali kwa kuwasaidia wananchi wa kawaida kisiasa, uchumi, na kijamii.
“Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka
yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine
maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu” uk.7. Uzalendo na ujasiri.
Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda nchi yake na kujitoa kuipigania katika mambo
mbalimbali yanayokwamisha maendeleo. Mwandishi anasema “pigano la kufa na
kupona lilikuwa mbele yake” uk.8. “alikuwa hana silaha nyingine za kuokolea
maisha ila zana hizi” uk.9. “Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake, siwezi
kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa Kitambo nikajinyima ushirika wa milele
unaotazamiwa kutokea baada ya kushindwa kwa uongo”uk.9. Mwandishi amewatumia wahusika
Karama, Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Radhaa, Amini kuonesha ujasiri na
uzalendo walijitoa na kufanyakazi katika masahibu mengi tena bila ya kukata
tama huku baadhi wakiishia kifungoni. Hatimaye waliweza kushinda. Mwandishi
anasema “kwa kazi zake bora na uaminifu mwingi hakushukuriwa bali kuvunjiwa
kadiri, aliaibishwa kuwa alileta uzushi ulikuwa hauna faida katika nchi zaidi
ya hayo alitumbukizwa katika kifungo cha maisha” Ujinga. Hali ya watu kutoelewa
mambo mbalimbali ya msingi kijamii kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi. Mfano haki
sheria na uongozi nakadhalika. Shaaban Robert amethibitisha uwepo wa ujinga
katika nchi ya kusadikika kupitia viongozi na wananchi waliosadiki mambo yao na
kuyakana ya nje. Pia mwandishi amewatumia wananchi waliohudhuria mahakamani
siku ya kwanza ya mashitaka. Msanii anasema “Baadhi ya watu wachache waliokuja
barazani kusikiliza kesi hii walimsikitikia mshitakiwa wengi walikuwa
wakinong’onezana kuwa msiba wa kujitakia hauna kilio” uk 7. “ujinga wao
haukuyazuia maendeleo tu lakini hasa ulirudisha nchi nyuma vilevile” uk. 14.
“Twaona kuwa mshitakiwa hana hatia ila alikuwa akitafuta jinsi ya kuisaidia
sheria ya kusadikika kwa njia ngeni” Maelezo haya ni matokeo ya ufumbuzi wa
ujinga uliokuwa umekithiri kwa viongozi wa kusadikika na wananchi wake. Uonevu
na Ukandamizaji (kukosekana kwa haki). Hali ya kutothaminiwa, kupewa haki na
kuhukumiwa bila ya kufanya kosa lolote, na wakati mwingine kutopewa nafasi ya
umuhimu katika tabaka fulani la watu “sheria za kusadikika zilikuwa hazimuamuru
mtu yeyote kujitetea juu ya ushahidi wa mshitaki” uk.7. Buruhani, Fadhili,
Kabuli, Auni, Radhaa, Amini walifungwa tena kwa kunyanyaswa Mwandishi anasema
“Natoa amri watu sita waliotajwa wafunguliwe mara moja, inasikitisha sana kwa
dhuluma juu ya watu hawa hazikutengenezwa mpaka leo. Gereza ni makao ya
wahalifu na watu hawa si wahalifu” Mhusika mkuu karama pia alishitakiwa na
Waziri majivuno kwa hulka tu za ukandamizaji. Umaskini. Ni hali ya kutomudu
kujipatia mahitaji mbalimbali ya kila siku kwa kiwango kinachoridhisha (cha
kutosha) Mwandishi anasema “kwa kukosekana kwa Madaraja mito inafanya shida juu
ya watu walio ng’ambo moja kukutana na Ng’ambo nyingine, maradhi hayajapata
uuguzaji, vifo vya mapema hapa katika mwaka mmoja jumla yake yatisha kuliko ile
ya vifo vitokeavyo katika nchi nyingine katika karne moja” Uk. 25. Pia
“Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka
yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine
maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka salama ya watu
wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi ya kusadikika” uk. 7. Maelezo haya
yanaonesha uwezekano mkubwa wa uwepo wa kundi kubwa la watu masikini ambao ndio
walioguswa na sheria za kusadikika.
Dhamira nyingine ndogondogo zilizomo katika
riwaya hii ni tamaa iliyooneshwa kupitia Salihi na Majivuno, Unafiki na woga wa
wananchi wa kusadikika, utengano na kukosekana kwa umoja. Migogoro. Hali ya
kutoelewa au kuridhishwa na jambo fulani na kupelekea kutoelewana kwa makundi
au pande mbili za watu. Katika riwaya hii kuna migogoro ya kijamii, kisiasa na
kiuchumi. Migogoro ya kijamii. Mfano wa migogoro ya kijamii ni mgogoro wa Sapa
na Salihi uliotokea baada ya Sapa kuomba upofu kutokana na tama ya Salihi
kutamani vitu vya Sapa, Mwandishi anasema “kwa sababu hii tuliafikiana
kushirikiana kila kitu atakachoomba tukaandikiana hati mbele ya Kadhi. Palepale
mwenzangu aliinua mikono yake juu akaomba upofu” uk.30 Mgogoro nafsia: ni hali
ya mtu kuhofia jambo fulani na kupelekea mtu huyo kuwa namsongo wa mawazo,
Mwandishi amemtumia waziri Majivuno aliyekuwa na hofu ya kupoteza madaraka na
kukomeshwa kwa ukandamizaji endapo wananchi wataelewa sheria mbalimbali za
kusadikika waliokuwa wakielimishwa na Karama. Hatimaye aliamua kumshitaki
katika baraza msanii anasema “Upelelezi huo ulidhihirisha bila ya shaka yoyote
kuwa mshitkiwa akiwafunza watu sio kuomba msamaha na huruma katika baraza tu
lakini hata kuzibatilisha hukumu za baraza la kusadikika kwa njia zote hii
inaonesha kuwa mgogoro mkubwa utakuwako kati ya sheria za nchi na watu wake” uk
2. Migogoro ya Kiuchumi. Mgogoro wa walionacho/matajiri ambao ndio waliopewa
haki na upendeleo na Maskini walionyimwa haki hata mbele ya sheria na
mahakaka.Katika nchi ya kusadikika watu hawa hawakuweza kabisa
kushirikiana.Mwandishi anasema “Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya
swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto
wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu.
Hapana shaka salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi ya
kusadikika” uk. 7. Migogoro wa Kisiasa. Huu ni mgogoro unaowahusisha
wanaharakati wazalendo walioongozwa na karama dhibi ya serikali na viongozi wan
chi ya kusadikika. Wanaharakati hao walihitaji mabadiliko na walichoshwa na
uonevu wa viongozi wao, mgogoro huu ndio uliopelekea wananchi kuishia kifungoni
pindi walipojitolea kudai mabadiliko. Ujumbe. Uongozi mbaya unachangia kwa
kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya wananchi. Kuwepo kwa hali ya uzalendo
katika nchi ni chachu ya maendeleo na mafanikio katika jamii. Suala la
uelimishaji (elimu) ni muhimu katika utambuzi wa wananchi katika shughuli
mbalimbali za kijamii.Tamaa na viongozi kujali maslahi kunapelekea hali duni ya
wananchi walio wengi. Viongozi wanapaswa kuthamini haki za wananchi
wanaowatumikia. Msimamo wa Mwandishi. Msimamo wa mwandishi katika riwaya hii ni
wa kimapinduzi kwani anaonesha jinsi jamii ilivyopaswa kujituma tena kwa
ujasiri, kupigania haki na mabadiliko ya wananchi wote. Mtazamo wa Mwandishi.
Mtazamo wa mwandishi wa riwaya hii ni wa Kiyakinifu kwani kwa kiasi kikubwa
umeakisi mambo ambayo yanaweza kufuatwa katika kufanikisha maendeleo ya jamiii
yeyote kama vile mgongano wa mawazo uzalendo na ujasiri, uelewa na mambo
mengine. Aidha yapo baadhi ya maeneo yanagusia mtazamo wa kidhanifu kama vile
kusadiki kila kinachosemwa na watawala. Falsafa ya mwandishi. Falsafa ya
mwandishi ni ya wema hushinda ubaya, amedhihirisha hili kupitia mhusika Karama
aliyechorwa kama mtu mwema dhidi ya Majivuno aliyechorwa kama mtu mbaya. Kwa
taswira hii Karama amewakilisha wema wote katika jamii ya wasadikika na
Majivuno anawakilisha wabaya wote katika jamii hiyohiyo.
MWISHO WA KITABU.
kazi nzuri
ReplyDelete